WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk. Mary Nagu pamoja na Mbunge wa Babati Vijijini, Jitu Soni (CCM), wamenusurika kuchomwa moto na wafuasi wa Chadema usiku wa kuamkia jana.
Tukio hilo lilitokea usiku wa manane, baada ya wafuasi wa Chadema, wakiongozwa na Mbunge wa chama hicho Jimbo la Karatu, Mchungaji Israel Natse, kuvamia nyumba waliyokuwa wamefikia Nagu na Soni, katika Kata ya Bashnet, Babati Vijijini, mkoani Manyara.
Wafuasi hao wa Chadema wanawatuhumu Dk. Nagu na Soni kukutana katika nyumba hiyo kwa nia ya kupanga mipango ya kutoa rushwa ili kufanikisha uchaguzi mdogo wa udiwani katika Kata hiyo, unaotarajiwa kufanyika leo, ikiwa ni pamoja na maeneo mbalimbali nchini.
Chanzo cha MTANZANIA Jumapili kilichokuwa eneo la tukio kililidokeza kuwa Dk. Nagu na Soni
walikwenda kijijini hapo usiku, wakiwa na magari mawili, kila mmoja na lake na kufika nyumbani kwa mtu aliyetajwa kwa jina la Petro Baha, kwa kile kilichodaiwa kuwa ulikuwa ni mpango wa kupita na kugawa fedha kwa wananchi usiku huo, ambapo pia inadaiwa ndani ya nyumba hiyo alikuwepo mgombea udiwani wa Kata hiyo, Nicodemus Gwandu (CCM).
Kitendo cha Nagu pamoja na Soni kuonekana katika nyumba hiyo kiliwashitua wafuasi wa Chadema, ambao baada ya muda mfupi walivamia nyumba hiyo wakiwa na Mbunge wao, Natse, madiwani na msafara wa pikipiki na kutishia kuichoma moto.
“Kilichotokea saa 7 usiku tulipigiwa simu na wananchi kuwa Waziri Nagu na Soni walikuwa eneo la Bashnet, ambalo ndiyo ngome yao ya rushwa na walikwenda kugawa huko, lakini walipoonekana tu yowe lilipigwa na watu walikusanyika wakitoka na silaha, ikiwemo mapanga na mikuki,” alisema.
Mtoa habari huyo alisema kuwa, wafuasi hao wa Chadema waliweka kambi katika nyumba hiyo kuhakikisha Nagu na Soni hawatoki kwenda kwa wananchi usiku huo.
Chanzo kilisema kitendo cha kuzingirwa huku wakitishia nyumba kuchomwa moto kiliwashitua viongozi hao wa CCM na kuamua kupiga simu polisi, ambao walifika wakiwa sita muda mfupi baadaye kwa ajili ya kuimarisha ulinzi hadi walipotoka jana asubuhi.
Inaelezwa kuwa mgombea wa udiwani wa CCM, Nicodemus, ambaye naye alikuwemo ndani ya nyumba hiyo pamoja na akina Nagu, yeye alifanikiwa kutoroka mapema kwa kuruka ukuta na kukimbia.
Alipotafutwa Dk Nagu ili kupata ukweli kuhusu taarifa hizo, simu yake ya kiganjani iliita bila mafanikio na hata alipotumiwa ujumbe mfupi nao hakujibu.
Habari kwa hisani ya mpekuzi.
TUPE MAONI YAKO HAPA:
0 comments:
Post a Comment