WAKATI wa kujadili na kubadilishana mawazo juu ya maisha ya uhusiano wa kimapenzi umewadia tena rafiki zangu. Naendelea kuwashukuru wasomaji wangu ambao mmekuwa mkinipa moyo kwa kuwasiliana nami kwa  njia ya SMS, waraka pepe na hata kwa kunipigia simu.

Bila shaka mada ya leo itawagusa zaidi wanandoa wa jinsia zote bila kujali itikadi zao. Kwa moyo mkunjufu nawakaribisha mfungue akili zenu kwa ajili ya kuingiza kitu kipya.

Hapana shaka kila mwanandoa anajua maana ya nyumba ndogo! Kwa faida ya wengi, nyumba ndogo ni mwanamke aliyewekwa kimada na  mwanaume aliyeoa huku akihuhudumiwa kwa hali na mali na kutimiza shida za ndani za mwanaume huyo.

Wanawake hawa, hugharamiwa kila kitu na waume za watu huku asilimia kubwa wakijua wazi kwamba wanaume walionao ni waume za watu. Nimesomeka?

Sasa twende kwenye mjadala kamili. Watu wengi (hasa wanawake walio ndani ya ndoa) hujiuliza sababu za waume zao kutafuta nyumba ndogo wakati wakiamini kwamba wao ni wazuri na wanawatimizia kila kitu ndani; kwa nini wanatoka nje?

Haya yamekuwa maswali ambayo yaliyokosa majibu. Wakati mwingine mtu anayejua kwamba mwanaume fulani anahudumia nyumba ndogo, wakati mwanaume huyo ana mke  mzuri ajabu, anafuata nini huko?
Chanzo cha kuamua kuandika mada hii ni simu mbalimbali za wasomaji wangu wakilaumu kuhusu waume zao kutoka nje ya ndoa.

Kuna dada mmoja nilimsikia akisema: “Mwanaume hata umfanyie nini hawezi kutulia ndani ya nyumba na mkewe.” Sijui kama ni kweli.

Kwangu mimi nimeona nisogee hatua moja mbele zaidi kwa kujiuliza, tuwaaache wanaume watoke...lakini kwa nini wanatoka? Kwa nini wanamiliki nyumba ndogo? Kuna nini huko nje ambacho wanakikosa ndani ya nyumba zao? Naamini kwa kujua hilo, inaweza kusaidia kufahamu nini cha kufanya ili watulie ndani ya nyumba zao.

Sasa twende pamoja tukaone.
Uhuru zaidi....!
Wanaume wanapenda kuwa uhuru kwa wake zao lakini kwa bahati mbaya wanawake wengi walio ndani ya ndoa hawapendi au huogopa kuwafanya waume zao kuwa huru!

Pengine naweza kuwa nimekuacha kidogo, usijali, nitakuweka sawa. Uhuru ninaozungumza hapa ni mpana sana. Namaanisha uhuru na mwili wako, nikisema hivyo namaanisha wanaume wanataka kuachiwa huru katika kufanya michezo ya kimapenzi na wake zao.

Mwanamke akishaolewa, anajifanya ana heshima sana, hata akitoka bafuni, akitaka kubadilisha nguo chumbani akiwa na mumewe tu, atavaa na khanga au taulo juu yake. Unaficha nini?

Hataki kuoga na mumewe, hana muda wa kupiga naye stori, watu wanaishi nyumba moja lakini wanaogopana. Utakuta mwanamke anachokijua yeye ni kumwambia mumewe: “Za saizi baba Jully,” baada   ya hapo ndiyo amemaliza tena.

Mwanamke unatakiwa kubembeleza, mpe uhuru mumeo, mfanye kama mtoto mdogo, adeke mbele yako. Sasa dada zangu, niwamegee siri, huko kwenye nyumba ndogo, wanajua sana kuhakikisha kipengele hicho kinakamilika!

Wanajua kubembeleza, wanatoa uhuru kwa wenzi wao, kiasi kwamba mwanaume anaona kero kuwa na mkewe. Kumbuka kwamba wakati akitoka nje, si kwamba hakupendi, anakupenda sana lakini kuna kitu cha ziada anakitafuta!
Utundu zaidi...

Mwanaume anapenda kufurahia mapenzi na mkewe kikamilifu lakini tatizo linakuja pale mwanamke anapokuwa hafahamu majukumu yake vizuri awapo faragha!

Mke anaogopa kuonesha utundu zaidi kwa mumewe akidhani ataonekana malaya...siyo kweli dada zangu. Sasa kutokana na woga huo, ndiyo maana waume zenu wanaamua kwenda nje ambapo watafaidi kwa raha zao.

Wakati mwingine mke anajua utundu wote kuhusu faragha, anajua mitindo chungu nzima ambayo inaweza kumpagawisha mumewe lakini anazubaa kwa madai eti anaogopa! Sasa hapo ndipo unapotoa mwanya wa kuzikaribisha nyumba ndogo!

MKE SI UZURI WA SURA!
Rafiki zangu kuna wake wanaojidanganya na uzuri wa sura na muonekano wao wa nje. Kwamba nini kinachosababisha waume zao watoke wakati wao ni wazuri?

Dada yangu mpenzi, uzuri wako si tija. Lazima ujue majukumu yako kama mke, uwe na kauli tamu ya kumbembeleza mumeo, mpokee kwa maneno mazuri, mpe pole anapotoka kazini, weka nyumba katika hali ya usafi, ulimi wako daima unakuwa mtamu, si utamu wa sukari, hapa namaanisha utamu wa kupima maneno yako kabla hujamtamkia mumeo.

Unaweza kumtafuta mchawi wa ndoa yako miaka nenda rudi lakini usipate, kumbe mchawi ni wewe mwenyewe.
Starehe zaidi...

Wakati mwingine, wanaume hushawishika kwenda nje ya ndoa zao kwa ajili ya kusaka sterehe zaidi. Kipengele hiki naomba kieleweke vizuri kwamba, mwanaume anatafuta starehe kwa maana ya kutaka kufanya ngono isiyokubalika!

Hii haikubaliki mahali popote pale, maana inaonekana wanaume wengi wanaomiliki nyumba ndogo, huwaruka ‘ukuta’ wanawake hao. Hapa kuna pande mbili,  nyumba ndogo zenyewe huwafundisha wanaume ‘kamchezo hako’ wakiamini kwamba watawashika na hawataweza kuwaacha kabisa.

Lakini pia wanaume wengine wakishakolea kwenye tabia mbaya ya kutoka nje, hujifunza au kusikia habari za mchezo huo mchafu na mwisho wa siku wanaamua kuwaomba ‘nyumba’ ndogo zao wafanye nao upuuzi huo huku wakiwaambia kama kweli wanawapenda basi wawatimizie!

Ni kweli kwamba, si rahisi kumwambia mkeo juu ya mchezo huu hatari kiafya na usiokubalika na imani mbalimbli, hivyo kwa kutafuta njia ya mkato,  mume anaamua kuucheza kwa nyumba ndogo yake!

“Ni zaidi ya miezi sita sasa ananilazimisha aniruke ukuta kwa ahadi ya kuninunulia gari la kutembelea lakini namzungusha. Amekuwa mnyonge sana siku hizi akisisitiza kwamba kama nikikubali nitakuwa nimeonesha mapenzi yangu ya dhati kwake.

“Ila juzi nilimuuliza kama kwa mkewe huwa anafanya hivyo, akabaki kimya...hakuwa na jibu kabisa! Yaani pamoja na tabia yangu ya kutoka na mume wa mtu, lakini sitarajii kabisa kufanya kitendo hicho kichafu katika maisha yangu,” anasema Leila, mfanyakazi wa Saluni moja ya kike iliyopo Kimara Baruti ambaye alikiri kutoka na mume wa mtu katika mazungumzo nami kwa njia ya simu.

Kifupi si mchezo mzuri kwani huathiri mfumo mzima wa njia ya haja kubwa, mwisho wa siku choo huweza kutoka bila taarifa au kupata tabu wakati wa kujifungua. Kwa ujumla wanawake wote wenye kufanya mchezo huu, wanatakiwa kuacha kabisa.

Je, kuna nini kingine kinachosababisha waume za watu wazichangamkie nyumba ndogo? Wiki ijayo si ya kukosa katika mwendelezo wa mada hii.

Tutaona kwa kirefu mambo hayo na vitu vya kuzingatia ili wanaume watulie kwenye ndoa zao. Ahsante sana kwa kunisoma, kazi kwenu kuyafanyia kazi haya machache niliyoyabainisha hapa.
TUPE MAONI YAKO HAPA:
LIKE PAGE YETU ILI UPATE HABARI ZAIDI

0 comments:

Post a Comment