MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto amesema atatembea na kuhutubia mikutano ya hadhara ya wananchi nchi nzima bila kuogopa wala kukatazwa na mtu.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara kwenye viwanja vya Mwanga Centre mjini hapa jana, Zitto alisema hazuiwi na maneno ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willbrod Slaa aliyotoa mkoani Tabora kwamba mikutano anayofanya nje ya jimbo lake ni kinyume cha Katiba.

Alisema akiwa mwanachama hai wa Chadema na mbunge, ana haki ya kutembea na kuhutubia mikutano ya hadhara mahali popote na kudharau maneno yaliyotolewa na Dk Slaa kwamba ni kama kelele za chura hazimzuii tembo kunywa maji.
Zitto aliongeza kuwa Dk Slaa ametoa maneno ya kutaka watu “waniambie niache kuhutubia mikutano hiyo kwa sababu inaweza kusababisha mimi kufukuzwa chama,” jambo ambalo kwake yeye amebainisha kama wanatoa hukumu. “Wamenipa siku 14 kutoa utetezi wangu, kwanini wasinifukuze chama, siku hizo zimeshakwisha lakini hawataki kukutana kutoa uamuzi, badala yake kila kiongozi anatembea mikoani kivyake na kutoa maneno ya kunihukumu,” alisema Mbunge huyo.
Aidha, alituhumu uongozi wa Chadema kumzushia uongo kwamba anahamasisha wajumbe wa Baraza Kuu kuomba mkutano kujadili suala la zima wakati wanaoomba hayo ni viongozi ambao wako madarakani chini ya viongozi wa Chadema, makao makuu na si chini yake.
Alisema mapokezi anayopata katika majimbo ya Mkoa wa Kigoma yanawatia kiwewe viongozi wa chama hicho na ndiyo maana wanatoa maneno ya kutaka kumwonesha kwa wananchi kuwa kiongozi asiyefaa.
Wananchi wanajua utendaji wangu, wanajua kazi kubwa niliyofanya kwao ndiyo maana kila ninakokwenda wanakuja kwa wingi kusikiliza nawaeleza nini, waniache niwaeleze wananchi kinachoendelea wasiwazuie hawana uwezo huo,” alisema Zitto.
Katika hatua nyingine, mbunge huyo alisema anatafuta ushauri wa kisheria aweze kusajili jina jipya la Mwami Ruyagwa alilotawazwa na wazee wa Wilaya ya Kasulu alipokuwa kwenye ziara ya mikutano ya hadhara wilayani humo.

Source: Habari Leo
TUPE MAONI YAKO HAPA:
LIKE PAGE YETU ILI UPATE HABARI ZAIDI

0 comments:

Post a Comment