Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema mwanachama wake yeyote atakayeshawishiwa kuuza kadi ya chama hicho kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) afanye hivyo, lakini asikubali kuiuza chini ya Sh. 100,000.
Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk.Willibrod Slaa, akizunguma na wananchi wa kijiji cha Tula jimbo la Igalula wakati wa ziara yake ya wiki tatu ya kuimarisha chama katika mikoa ya Tabora, Kigoma na Singida, alisema kadi hiyo ikiuzwa kwa kiwango hicho zitamsaidia kupata fedha za kuanzishia mradi wa biashara.
“CCM wamewanyima ajira kwa hiyo mtu akija anataka kununua kadi ya Chadema ruksa kumuuzia lakini msiuze chini ya Sh. 100,000 ili mpate fedha za kuanzishia biashara, mkiuza kwa Sh.1500 haitawalipa,” alisema.
Alisema wakati wa uchaguzi mkuu wa 2010, serikali ya CCM ilitangaza ajira 100,000 kwa vijana, lakini hadi sasa utekelezaji wake haupo na katika hali ya kushangaza ajira hizo zimejumuishwa hata za wabeba mikokoteni.
Katibu Mkuu katika baadhi ya majimbo ya mkoa wa Tabora alitoa ofa kwa kuwanunulia kadi wanachama wapya zaidi ya 4,000 katika majimbo ya mikoa ya Tabora na Singida.
Dk. Slaa akizungumzia amani alisema hivi sasa nchi inapitia katika kipindi kigumu sana kutokana na matukio ya kutisha yanayotokea maeneo mbalimbali hali inayotokana na wananchi kukata tamaa.
“Nchi ipo katika wakati mgumu wananchi wameanza kukosa uvumilivu kwa manyanyaso ndiyo maana mara utasikia wananchi wamevamia kituo cha polisi kwa lengo la kutaka kumtoa mtuhumiwa aliyekamatwa pengine kwa kuonewa,” alisema.
Alisema Tanzania mtu asiyekuwa na pesa amekuwa kama kuwepo kwake hapa duniani ni dhambi na mwenye pesa anaamua kufanya lolote kwa asiyekuwa na pesa.
TUPE MAONI YAKO HAPA:
0 comments:
Post a Comment