Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibroad Slaa, jana alianza rasmi ziara katika Mkoa wa Kigoma, huku akisema Chadema haiogopi chochote sababu ni chama cha demokrasia na chama cha kidemokrasia hakimuogopi Dk. Slaa, Mtei, Mbowe wala Zitto, bali kinaogopa katiba tu.
Aidha, alisema watu wanaoona waliingia ndani ya chama hicho kwa kumfuata, Zitto, aliyevuliwa wadhifa wa unaibu katibu mkuu waondoke naye wakasaidiane kuanzisha chama chao.
“Kama ambavyo mkristo ataheshimu Biblia na yaliyopo ndani ya Biblia, lazima yafuatwe na kwa Waislamu wanafuata Koran, kwa hiyo na sisi Chadema tunafuata katiba yetu,” alisema.
Alisema hayo wakati akizungumza na mamia ya wananchi wa mji wa Kakonko ambao ni makao makuu ya Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma.
Dk. Slaa alilazimika kusema hayo baada ya vijana wanne kuingia na mabango kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Mwenge mjini Kakonko yakiwa na ujumbe mbalimbali.
Alisema kama kuna watu wanafikiri chama ni mtu ruksa waende naye kwenye chama ambacho wanakitaka.
“Kama mnafikiri Zitto ni mkombozi wa Kakonko au Kigoma, basi awakomboe kwa chama atakachokianzisha msaidieni aanzishe chama chake kitakachowakomboa,” alisema.
Alisema: “Chadema ina utaratibu wake, ina katiba yake, ina muundo wake, hivyo kimekomaa, kinaendeshwa kwa katiba, hakiendeshwi kwa mabango.”
Alisema vijana wanaobeba mabango wanafikiri kuwa wamandaidia Zitto bila kujua kuwa wanamharibia.
Aliongeza kuwa ziara yake katika mkoa wa Kigoma hakuipanga kwa sababu ya Zitto, bali aliipanga tangu Julai kutokana na mikoa ya Kanda ya Magharibi kukabiliwa na matatizo ya manyanyaso ya kutisha wanayofanyiwa wananchi na polisi na vyombo vingine vya dola.
Dk. Slaa aliwashambulia vijana hao waliokuwa na mabango kwamba walipangwa kufanya hivyo baada ya kununuliwa gongo na kwamba kulikomboa taifa kwa vijana kama hawa ni kazi kweli.
“Nikiomba polisi wa Kakonko waje hapa wawapime kiwango chenu cha ulevi mpo tayari, kwanza hakuna atakayepona hapa,” alisema.
Hata hivyo, kati ya vijana wanne, mmoja ndiye aliyekubali baada ya kuhojiwa.
Dk. Slaa alipowahoji vijana hao wanatoka tawi gani la chama, lakini walishindwa kujieleza na hawakuwa na kadi wala hawafahamu hata wenyeviti wa matawi ya chama.
Baadaye walipojitambulisha, mmoja wa vijana hao aliyefahamika kwa jina la Shukuru Mbaga ilibainika kuwa ni mtoto wa Katibu Mwenezi mstaafu wa CCM na alikiri kuwa ni baba yake.
Vijana hao waliingia na mabango saa 8:50 alasiri kwenye viwanja vya Mwenge wakiwa na mabango hayo yenye ujumbe mbalimbali.
Mabango hayo yalikuwa na ujumbe kama “Kigoma bila Zitto haiwezekani”, “Hatupo tayari kukusikiliza kwa lolote”, “Zitto mkombozi wana-kigoma, Tanzania, Kakonko”, “Bila Zitto haiwezekani” na “Mhe. Slaa na Mhe .Mbowe nyote mnatakiwa kijiuzulu mara moja”.
Awali Dk. Slaa alianza ziara yake mkoani Kigoma kwa kuzungumza na wananchi wa kijiji cha Muhande wilayani hapa katika mkutano wa hadhara na kuhutubia mkutano uliohudhuriwa na wananchi wengi.
Baadaye alikwenda mjini Kakonko na msafara wake kupokelewa na vijana waliokuwa na mabango manne wakati akiingia katika viwanja vya Mwenge kuhutubia wananchi.
Hata hivyo, vijana hao walipata wakati mgumu baada ya kuzuiliwa na polisi pamoja na walinzi wa chama hicho wakati wakiingia katika viwanja wakiwa na mabango.
Dk. Slaa kabla ya kuanza kuhutubia wananchi alizuia polisi na walinzi wa chama wasiwakataze vijana hao na kutaka wawaruhusu kuingia katika viwanja na mabango hayo, jambo ambalo lilitekelezwa.
CHADEMA HAITAYUMBA
Awali akizungumza na wananchi wa Kata ya Muhande katika mkutano wa hadhara uolifanyika viwanja vya Shule ya Msingi Muhande, alisema Chadema haitayumba milele licha ya hujuma inazofanyiwa na wapinzani wake.
Alisema Chadema haiwezi kuyumba kwa sababu inajikita katika misingi yake na wala haingozwi kwa matakwa ya viongozi bali kwa kuzingatia katiba.
“Chadema haiongozwi kwa matakwa ya Dk. Slaa wala Mbowe, bali kwa matakwa ya katiba, kwa hiyo kamwe haitayumba milele kwani kila jambo tunalofanya tunamtanguliza Mungu na kumaliza na Mungu,” alisema.
Dk. Slaa alisema zipo kampeni kubwa zinafanywa kuichafua Chadema na hata kabla ya ziara yake mkoani Kigoma yapo maneno mengi ambayo yalisemwa ikiwamo kwamba yeye (Dk. Slaa) amepigwa marufuku kufanya ziara.
Alisema hakuna mtu anayeweza kumzuia asifanye ziara katika mkoa wa Kigoma na mikoa mingine kwa sababu Tanzania bado hatujafikia hatua ya mtu kuzuwiliwa kufika katika mkoa wowote.
Akizungumza juzi mjinni Kahama, mkoani Shinyanga, Dk.Willbroard Slaa, alisema chama hicho kinafanya kazi na kutoa maamuzi kwa kuzingatia katiba na kama wapo watu wanaotaka kuwa na chama legelege yupo tayari kuachia ngazi nafasi ya ukatibu mkuu.
Aliuambia umati wa wananchi katika viwanja vya CDT kuwa: “Chadema tuliahidi tutairudisha nchi kwenye mstari, kurudisha reli, lakini yote huwezi ukayarudisha ukiwa legelege, hatuhitaji chama legelege na kama mnasema tuwe na chama legelege hata ukatibu huu nipo tayari kuuacha.”
Alisema Chadema ni chama makini ambacho kinaunganisha na katiba, hivyo mtu yeyote asifikilie ni mkubwa kuliko katiba.
“Hata mimi na Mbowe (Mwenyekiti wa Chadema Taifa) katiba inatuwekea mipaka, kuna vitu ambavyo mimi kama katibu siwezi kuvisema, ni lazina visemwe na mwenyekiti wangu tu,” alisema.
Dk.Slaa alisema yanayoendelea ndani ya Chadema kwa sasa yamepangwa na chama tawala kama ambavyo walishawahi kusema baadhi ya mawaziri wa serikali ya CCM kwamba Chadema itakufa kabla ya 2013, lakini ni propaganda itavuka.
Aliongeza kuwa mambo mengine yanayoendelea hivi sasa ndani ya Chadema Watanzania waiachie Kamati Kuu ambayo ina watu makini wataweza kulipatia ufumbuzi tatizo lililopo.
TUPE MAONI YAKO HAPA:
0 comments:
Post a Comment