KIFO cha aliyekuwa mpiga ngoma (tumba) maarufu wa Bendi ya The African Stars ‘Twanga Pepeta International’, Soud Mohamed ‘MCD’ kimeacha simulizi inayouma, Amani linalia sanjari na ndugu.
MCD ambaye Agosti 4, 2013 alimpoteza baba yake mzazi, alifariki dunia usiku wa kuamkia Januari 28, mwaka huu katika Hospitali ya Kilimanjaro Christian Medical Center (KCMC) baada ya kusumbuliwa na maradhi kwa muda mrefu.
Simulizi inayouma ya mwanamuziki huyo ilianzia mwishoni mwa mwaka jana ambapo akiwa na bendi yake katika ziara ya kikazi mikoa ya Kanda ya Ziwa, wakati wa kurejea Dar, MCD aliuomba uongozi umruhusu aende nyumbani kwao Majengo Moshi, Kilimanjaro kupatiwa matibabu na kuwa karibu ya uangalizi wa ndugu zake.
Akizungumza na gazeti hili juzi, Meneja wa Twanga Pepeta, Hassan Rehani alisema uongozi ulimruhusu MCD kwenda kwao na kumuahidi kuwa naye karibu kwa kila hatua.
“Tulimkubalia kwenda kwao, lakini tulikuwa tukifuatilia hali yake kila siku,” alisema Rehani.
Rehani alisema: “MCD tulikuwa tukiwasiliana naye kujua hali yake, kabla ya usiku huu kupata taarifa za kifo chake watu wa hapa ofisini walizungumza naye vizuri tu mchana wake.”
Chanzo kingine kimeweka bayana simulizi hiyo inayouma kwamba, Jumatatu iliyopita, marehemu MCD alituma ujumbe kwa uongozi akisema hali yake haiendi vizuri, hivyo viongozi wake waliamua kumtumia nauli siku ya Jumatatu ili arudi kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi.
“Maskini, pesa ya nauli aliipata ili arudi Dar Jumanne (iliyopita) lakini akiwa anajipanga kusafiri hali ikazidi kuwa mbaya, akakimbizwa hospitalini ambako alifariki dunia. Kwa hiyo nauli yake ikanunulia sanda,” kimesema chanzo hicho.
Kikaendelea: “Si ajabu angewahi kusema hali yake si nzuri akatumiwa nauli mapema, akaja Dar leo hii tusingekuwa tunalia.
Juzi Jumatatu baada ya kupokea habari za kifo cha mwanamuziki huyo, baadhi ya viongozi wa Twanga waliwapigia simu wanamuziki wa bendi hiyo na kukutana kwa ajili ya kupanga taratibu za safari ya kwenda Moshi.
Aprili 27, mwaka jana, MCD aliondoka Twanga Pepeta na kwenda kujiunga na Mashujaa Music Band kabla ya kurejea tena.
Marehemu MCD amezikwa jana kwenye Makaburi ya Njoro, Moshi. Ameacha mke na watoto wawili. Mungu ailaze pema peponi roho ya marehemu. Amina.
Wakati huohuo, taarifa za kifo cha msanii wa Kundi la Futuhi, Omary Majuto maarufu kama Mzee Dude zimelishtua Jiji la Mwanza na kuwafanya baadhi ya watu kukaa kwa mafungu kumzungumzia marehemu.
Kifo cha Mzee Dude, kilimtikisa pia msanii maarufu nchini, Kulwa Kikumba ‘Dude’ baada ya baadhi ya watu kudhani kwamba yeye ndiye aliyefariki dunia.
Dude alilazimika kuwapigia simu baadhi ya ndugu na marafiki na kuandika katika ukurasa wake wa Mtandao wa Kijamii wa Facebook kuwafahamisha kwamba yeye ni mzima wa afya njema.
TUPE MAONI YAKO HAPA:
0 comments:
Post a Comment