MAISHA ya mwanafunzi wa kike mwenye umri wa miaka 12, (jina tunalihifadhi), anayesoma darasa la tano Shule ya Msingi Bwanza, Wilaya ya Bunda, mkoani Mara, yako hatarini baada ya kurukiwa na samaki aina ya sato, kuingia sehemu ya siri na kukimbilia tumboni.
Tukio hilo limetokea Januari mosi mwaka huu, saa 11 alfajiri, wakati mtoto huyo akichota maji katika Ziwa Victoria ili aweze kumwagilia bustani ya nyanya, vitunguu iliyopo kandokando ya ziwa hilo.

Akizungumza na Majira, kaka wa mtoto huyo (jina tunalihifadi), mwenye miaka 31, alisema tukio hilo limewashangaza wakazi wa Kijiji cha Bwanza na vitongoji vyake.


Alisema mdogo wake alikuwa akichota maji katika ziwa hilo akiwa amechuchumaa ndipo samaki huyo anayedaiwa kuwa mwenye ukubwa wa nchi nne, aliruka kutoka majini, kuingia sehemu yake ya siri na kukimbilia tumboni.


"Mdogo wangu alifanya jitihada za kumvuta ili aweze kumtoa lakini alikimbilia tumboni na kuanza kupata maumivu makali,kutokwa na damu nyingi baada ya kuparazwa na miba ya
mgongo wa samaki huyo.


"Baada ya tukio hilo, alirudi nyumbani kwa shida akijivuta na kuugulia maumivu... alimweleza mama na ndugu zake juu ya mkasa huu, walimchunguza na kujaribu kuingiza mkono sehemu za siri wakidhani watampata lakini hawakufanikiwa," alisema.


Aliongeza kuwa, baada ya kumpeleka zahanati iliyopo kijijini hapo, hali yake ilizidi kuwa mbaya akilalamika maumivu makali tumboni ambapo familia inaamini tukio hili limetokana na imani za kishirikina hivyo waliamua kumtoa katika zahanati hiyo.


"Tulimpeleka kwa mganga wa kienyeji kijiji cha Amuyebe, wilayani Ukerewe... katika hali ya kawaida samaki hawezi kumrukia mtu sehemu yake ya siri na kuzama tumboni.


"Pamoja na kuchukua uamuzi wa kumpeleka kwa mtaalamu, hali yake bado inazidi kuwa mbaya, hata baba yetu alifariki katika mazingira yenye utata mwaka 2003," alisema.


Aliongeza kuwa hata kaka zake watatu na mtoto huyo nao walifariki kwa mfululizo mwaka 2004, 2005, 2006 ambao vifo vyao viligubikwa na utata mkubwa.


Mwenyekiti wa Kitongoji cha Alwego anakoishi mtoto huyo, Bi. Reticia Bituro, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo ambalo limewashangaza watu na kuahidi uongozi wa kitongoji hicho utaendelea kufanya uchunguzi zaidi.


Diwani wa Kata ya Napindi, Bw. Elias Magoti ambaye yuko safari kuhudhuria kikao cha Baraza la Madiwani Bunda Mjini,alikiri kupokea taarifa za tukio hilo kwa mshangao mkubwa.


"Nitalifuatilia kwa karibu baada ya kurudi kijijini kwa kufanya uchunguzi ili kubaini kilichotokea kwani sijawahi kusikia tukio kama hili katika umri nilionao," alisema.
Taarifa zilizopatikana kutoka Ukerewe anakotibiwa mtoto huyo, zilisema kwa sasa hawezi kuzungumza akizidi kulalamika maumivu makali ya tumbo na samaki huyo bado hajatolewa. 


Chanzo: Gazet MAJIRA
TUPE MAONI YAKO HAPA:
LIKE PAGE YETU ILI UPATE HABARI ZAIDI

0 comments:

Post a Comment