MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, amesema atajiuzulu ujumbe katika Bunge Maalumu la Katiba na kwenda mahakamani kama wajumbe wenzake watakataa kuirejesha Tanganyika.

Mchungaji Mtikila aliyeteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwamo katika Bunge hilo, alisema kwa sasa anajiandaa kufungua kesi Mahakama Kuu kutaka kuvunjwa kwa Muungano na kudai katiba ya Watanganyika ambayo haipo.

“Nitawaeleza wajumbe wenzangu mambo ya msingi, ikiwemo Katiba ya Tanganyika kwanza, wakikataa najiuzulu ili niendelee na kesi yangu nitakayokuwa nimeifungua,” alisema.

Alisema jambo la muhimu ambalo lingefanyika kabla ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni uundwaji wa Katiba ya Tanganyika.

Mtikila alisema atashiriki kikamilifu katika Bunge hilo na atawaeleza wajumbe wengine jambo la kufanya kabla ya kupitisha rasimu ya katiba inayotarajiwa kujadiliwa kwenye vikao vitakavyoanza Februari 18 mkoani Dodoma.

Mbali ya Mtikila, baadhi ya wajumbe wengine waliochaguliwa kuunda Bunge hilo maalumu, wamesema watakwenda kutetea maslahi ya nchi kwa ajili ya Watanzania wote.

Kaimu Katibu Mkuu Kiongozi, Dk. Florence Turuka, kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete, juzi alitangaza majina 201 ya wajumbe watakaowakilisha Bunge Maalumu la Katiba wanaotoka katika makundi 10 nchini.
Makundi hayo ni taasisi zisizokuwa za kiserikali (NGOs), taasisi za kidini Tanzania Bara, vyama vya siasa, taasisi za elimu, watu wenye ulemavu, vyama vya wafanyakazi, vyama vinavyowakilisha wafugaji, vyama vya wavuvi, vyama vya wakulima na watu wenye malengo yanayofanana.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Tanzania Daima Jumapili, baadhi ya wateule hao waliwashauri wajumbe wenzao kuwa makini kwa kuwa katiba ndiyo sheria mama inayowaongoza wote, hivyo hawatakiwi kupeleka matakwa ya vyama vyao.

Naibu Katibu Mkuu (bara) wa Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro, alisema msimamo wa chama chao ni kuwakilisha wananchi huku akisisitiza kwamba wajumbe wa Bunge hilo wanapaswa kuachana na maoni ya vyama vyao kwa kuwa katiba ni mali ya taifa.

Wasomi wanena
Kwa upande wa wasomi na wanaharakati katika masuala ya kisiasa wamejitokeza kupongeza na wengine kupinga uteuzi wa majina 201 ya wajumbe watakaongia katika Bunge la Katiba litakaloanza wiki ijayo.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Profesa Mwesiga Baregu, alisema ingependeza kama majina hayo yaliyoteuliwa na Rais Kikwete yangerejeshwa kwa wananchi ili wachague wenyewe.

Aliongeza kuwa wananchi walipaswa wachague wajumbe wa kuwawakilisha kama ilivyo katika chaguzi za udiwani, ubunge na rais kwa kuwa hilo ni Bunge linaloenda kujadili maswala yao.
“Naweza kusema kwamba, uteuzi wa rais si mbaya sana kwa kuwa umechukua wawakilishi katika makundi yote… lakini ingependeza kama wananchi wangejichagulia wawakilishi wao kwa kuwa lile ni Bunge lao na si vinginevyo,” alisema msomi huyo.

Profesa Baregu ambaye alikuwa mjumbe katika Tume ya Mabadiliko ya Katiba itakayomaliza muda wake wakati wa kupiga kura ya maoni, alisema anatarajia wajumbe hao watawawakilisha vema wananchi kwa kuwa waliomo ni wanaharakati, wanasiasa kutoka katika vyama vya siasa vyote vyenye usajili wa kudumu.
Mhadhiri Mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, alisema uteuzi huo umezingatia sheria na kuangalia makundi yote ambayo yalitakiwa kuwa na wawakilishi.

“Nampongeza Rais Kikwete kwa kuzingatia sheria katika uteuzi wake, lakini pia amenifurahisha zaidi kuwachukua viongozi wote wa siasa ambao vyama vyao vina usajili wa kudumu kwenda kuifanya kazi ya wananchi waliowaamini,” alisema Dk. Bana.

Alisema anatarajia vongozi wa siasa ambao wamepata nafasi hiyo, wakiwa katika Bunge hilo watajifunza kujenga hoja, kuheshimiana na kuvumiliana ili watakapotoka hapo, waweze kuwa viongozi bora.
“Ni matumani yangu kuwa Bunge hilo litakapomaliza na rasimu hiyo kurejeshwa kwa wananchi, viongozi hao watatumia uzoefu walionao kuwaelimisha wananchi na wafuasi wao hoja zilizojadiliwa na kupitishwa ili kurahisisha upigaji kura ya maoni,” alisema.

Kabla ya kutangaza majina hayo, Dk. Turuka alisema kazi ya kuwapata wajumbe wa Bunge hilo ilikuwa ngumu kwani walioomba walikuwa 3,754 na waliotoswa ni 3,553.

Alisema wapo waombaji 118 waliojiteua wenyewe na kwamba kulikuwa na vimemo vya waliokuwa wakiomba uteuzi kinyume cha sheria.

Alisema uteuzi huo umezingatia ushiriki wa rika na jinsi zote na kwa kuzingatia uwiano wa theluthi moja ya wajumbe kutoka Zanzibar na theluthi mbili kutoka Tanganyika kwenye kila kundi.

Kwa mujibu wa Dk. Turuka, wajumbe vijana wenye umri kati ya miaka 22 hadi 35 wapo 35; wenye umri wa kati ya miaka 36 hadi 64 wapo 145 na wenye umri wa miaka 65 na kuendelea wapo 21.

“Hapa kwenye umri yupo mjumbe mwenye miaka 81, tulizingatia hilo kwa sababu uzee dawa… kati ya wote hao wapo wanawake 100 na wanaume 101 ili kuweka uwiano wa jinsia, japo kidogo kwa wanaume imezidi kwa sababu hakuna mtu nusu,” alisema. 
TUPE MAONI YAKO HAPA:
LIKE PAGE YETU ILI UPATE HABARI ZAIDI

0 comments:

Post a Comment