MBUNGE wa Mpanda Mjini, Said Arfi, jana aliwaaga wapiga kura wake akiwaeleza kuwa uanachama wake Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) utakoma mara baada ya kuvunjwa kwa Bunge la 10 mjini Dodoma.
Akizungumza katika
mkutano wa hadhara uliofanyika katika Shule ya Msingi Kashato mjini hapa
jana, Arfi, aliyekiwakilisha chama hicho kwa miaka 10 mfululizo,
aliwaambia wananchi kuwa jimbo hilo litakuwa wazi wakati wowote wiki
ijayo.
“Kama Chadema wana ubavu,
waje walikomboe jimbo hili. Mimi ninaifahamu Chadema kuliko mtu yeyote
mkoani Katavi kwani nilikuwa Makamu Mwenyekiti (Bara), na sasa
nitamuunga mkono yeyote anayefaa kuwa mrithi wangu,” alisema Arfi na
kushangiliwa.
Mkutano huo uliohudhuriwa
na umati mkubwa, ulikuwa chini ya ulinzi mkali wa polisi kutokana na
kuzagaa kwa taarifa za kutaka kufanyiwa fujo kwa Mbunge huyo na watu
wanaoaminika kuwa wafuasi wa Chadema.
Arfi alisema hatogombea
tena Mpanda Mjini; “Lakini nipo tayari kuvaa shati la kijani au la
zambarau kumpigia debe mgombea yeyote katika jimbo hili. Ninawajua
Chadema na kama wakiendelea kunifuatafuata, nitasema yote.”
Kauli hiyo ilitafsiriwa
kuwa Arfi sasa atafanya kampeni akiwa CCM au ACT Wazalendo dhidi ya
Chadema katika Jimbo la Mpanda Mjini, ambalo kabla yake halikuwahi
kutawala na Mbunge mmoja kwa miaka 10 mfululizo.
Hii ni mara ya kwanza kwa
Arfi kuweka hadharani mustakabali wake kisiasa, lakini kauli yake ya
kuwa tayari kuvaa shati la kijana inakwenda tofauti na fununu
zilizozagaa mjini hapa kuwa huenda akajiunga na ACT Wazalendo, chama
kinachoongozwa na swahiba wake, Zitto Kabwe.
Ikumbukwe kuwa mara baada
ya Chadema kutangaza kumvua nyadhifa zote Zitto takriban miaka miwili
iliyopita, mara moja Arfi alitangaza kuajiuzulu nafasi ya Makamu
Mwenyekiti wa Chadema.
TUPE MAONI YAKO HAPA:
0 comments:
Post a Comment