MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema), anatarajia kuanza ziara ya siku tano mkoani Kigoma, itakayomfikisha katika majimbo mbalimbali ya uchaguzi mkoani Kigoma.
Katibu wa mbunge huyo, Alex Kitumo alisema jana kuwa Zitto atawasili mkoani Kigoma leo ambapo atapokewa Uwanja wa Ndege wa Kigoma kwa maandamano ya wanachama na wapenzi wa mbunge huyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, maandamano hayo ya wanachama na wapenzi wa Chadema Mkoa wa Kigoma, yatamsindikiza mbunge huyo hadi eneo la Mwandiga kwenye ngome yake Kuu ambapo atahutubia mkutano wa hadhara.
Ziara hiyo ya Zitto, imeanza wakati mahasimu wake, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, wakifanya ziara kama hizo, zinazoitwa za kuimarisha chama.
Tofauti na jina la ziara hizo, kwamba ni za kuimarisha chama, viongozi hao wa Chadema wamekuwa wakiuuza uamuzi wa Kamati Kuu ya Chama hicho wa kumvua madaraka Zitto na wenzake.
Hata hivyo, Kitumo hakusema kama Zitto naye atatumia ziara hiyo kupinga akina Mbowe na Dk Slaa, lakini alisema siku inayofuatia, Zitto atakuwa na mikutano miwili wilayani Kasulu ambako kabla ya mikutano hiyo ya hadhara, atakuwa na kikao cha ndani na wazee wa Chadema wa wilaya hiyo kabla jioni hajahutubia mkutano wa hadhara mjini Kasulu.
Ratiba ya Mbunge huyo inaonesha kuwa baada ya mkutano wa Kasulu siku ya Jumatatu, Zitto atafanya mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Mkongoro Kigoma Vijijini jimboni kwake, mkutano ambao utatanguliwa na mkutano wa wazee wa jimbo hilo pia.
Katibu wa mbunge huyo alisema kuwa baada ya ratiba hiyo ya awali, watatoa ratiba nyingine ya shughuli za mbunge huyo mkoani Kigoma ambayo pia itazingatia majukumu yake mengine ya Kitaifa ya Mbunge huyo ambayo hayakuwekwa wazi.
Waandishi wa habari walitaka kujua kama Zitto anaruhusiwa kufanya mikutano maeneo mengine tofauti na jimboni kwake, wakati amevuliwa nyadhifa zote za chama kitaifa, lakini Katibu wa Mbunge alijibu kuwa Katiba ya Chadema inamruhusu kufanya hivyo.
“Katiba inampa mamlaka Zitto kama Mbunge ya kufanya shughuli ambazo atazifanya za kuimarisha chama na kusaidia chama chake na ndiyo dhamira kuu ya ziara hiyo,” alisema Kitumo.
Licha ya habari za ndani kueleza kuwa ziara hiyo inalenga kufuta propaganda zilizopandikizwa na Dk Slaa, Kitumo alikanusha jambo hilo na kusema kuwa ziara hiyo haihusu lolote kuhusu aliyozungumza au kufanya Dk Slaa.
---Habari leo
---Habari leo
TUPE MAONI YAKO HAPA:
0 comments:
Post a Comment