JESHI la Polisi mkoani Simiyu linamshikilia mwanamke na mkazi wa Kijiji cha Usiulize wilayani Meatu kwa tuhuma za kumuua mpenzi wake kwa kumvuta korodani, kutokana na wivu wa kimapenzi.
 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Charles Mkumbo alisema tukio hilo lilitokea juzi saa tisa usiku katika Kitongoji cha Mlimani Kijiji cha Usiulize Kata ya Mwamalole.
 
Alisema katika tukio hilo, wapenzi wawili Jumanne Gunda (39), mkazi wa Kijiji cha Kinyambuli wilayani Mkalamo, akiwa amelala na mchumba wake, Mariamu Khamis (49) mkazi wa Kijiji cha Ibaga Wilaya ya Mkalamo mkoani Singida, kulitokea kutoelewana kati yao na kusababisha wagombane.
 
Katika ugomvi huo, ambao chanzo chake ni wivu wa kimapenzi, Mariamu anatuhumiwa kuzivuta korodani za mpenzi wake na kusababisha mishipa muhimu kukatika na kusababisha kifo cha Jumanne papo hapo.
 
Kufuatia kifo hicho, Mariamu aliburuza mwili wa mpenzi wake mpaka chooni kwa lengo la kuutumbukiza katika shimo la choo. Hata hivyo kutokana na udogo wa tundu la choo, alishindwa kutumbukiza mwili huo chooni na hivyo kuamua kuutelekeza humo.
 
Asubuhi kulipopambazuka, majirani wa nyumba waligundua mwili wa marehemu ukiwa umetelekezwa chooni na kutoa taarifa Kituo cha Polisi, ambao walifika katika eneo la tukio na kumtafuta mtuhumiwa, Mariamu.
 
Baada ya Mariamu kukamatwa, anatuhumiwa kukiri kumuua mpenzi wake katika ugomvi kati yao, uliotokea usiku walipokuwa wamelala wote wawili. Anatuhumiwa kukiri kumvuta korodani zake na kusababisha kifo chake.

TUPE MAONI YAKO HAPA:
LIKE PAGE YETU ILI UPATE HABARI ZAIDI

0 comments:

Post a Comment