Ni Ally Awadh wa kampuni ya mafuta ya Lake Oil
Atuhumiwa kumfanyia unyama mtumishi wake
Polisi Oysterbay, Kanda Maalumu wamgwaya
Jumanne, Februari 11, 2014
Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ameamua “kujipima uzito” dhidi ya bilionea Mtanzania, Ally Edha Awadh ambaye ni mmiliki wa kampuni ya Lake Oil ya Mikocheni jijini Dar es Salaaminayoagiza, kuuza na kusafirisha mafuta na biashara nyingine nyingi. Awadh anayetajwa kama mmoja wa mabilionea vijana nchini, amefunguliwa mashitaka Polisi ya kumteka, kumdhalilisha kinyume cha maumbile na kumpora mali mmoja wa wafanyakazi wake.
Uamuzi wa Waziri Mkuu Pinda umekuja baada ya Jeshi la Polisi nchini, katika kile kinachoonekana ni kumgwaya bilionea huyo, kupuuza kumsaidia mlalamikaji huyo mwenye umri wa miaka 32. Kwa sababu za kiutu na za kitaaluma, jina la mlalamikaji tunalihifadhi kwa sasa.
Hatua ya Pinda imetokana na barua ya mlalamikaji ya Novemba 29, mwaka jana aliyomwandikia baada ya Jeshi la Polisi-kuanzia Kituo cha Oysterbay, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam na hata Makao Makuu, kupuuza kumsaidia mlalamikaji ili aweze kutendewa haki.
Baada ya kuipata barua ya mlalamikaji, Pinda alimwagiza msaidizi wake, Leila Mgonya, amwandikie barua Katibu wa Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Kazi hiyo ilifanywa Desemba 29, mwaka jana.
Katika barua hiyo ya Pinda iliyoandikwa kwa niaba yake na Mgonya, inasema, “Miongoni mwa mambo aliyofanyiwa mlalamikaji na mwajiri wake (Awadh) ni pamoja na kupigwa na kujeruhiwa mwili mzima kama picha zilizoambatanishwa na barua ya mlalamikaji zinavyoonyesha, kudhalilisha pamoja na kudhulumiwa mali zake kama inavyobainishwa katika barua ya mlalamikaji.
“Kwa kuwa suala hili limejikita zaidi katika utendaji wa Jeshi la Polisi, imeelekezwa kuwa, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ishughulikie suala hili kikamilifu kwa lengo la kumsaidia mlalamikaji kupata haki yake kwa mujibu wa sheria na kuona kuwa haki inatendeka.
“Aidha, Mheshimiwa Waziri Mkuu angependa kupata mrejesho kuhusu suala hili. Tafadhali mfikishie Mheshimiwa Waziri maelekezo hayo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.”
Pamoja na maagizo hayo ya Waziri Mkuu, JAMHURI imebaini kuwa hakuna hatua zozote za maana zilizokwishachukuliwa dhidi ya Awadh na washirika wake.

Barua ya mlalamikaji kwa Waziri Mkuu
Mlalamikaji katika barua yake kwa Waziri Mkuu, anaanza kwa kusema, “Mheshimiwa, jina langu lipo hapo juu ni kijana wa Kihidi (Mtanzania) umri wangu ni miaka 32 mzaliwa wa Tanga, nina mke na watoto.
“Mheshimiwa, nimesomea uhasibu na nimefuzu mwaka 2004 masomo yangu… na nikaajiriwa na Ally Edha Awadh katika kampuni yake iitwayo Lake Oil Ltd Septemba, 2010 na kuwa Finance Manager (Meneja Fedha) katika kampuni yake.
“Bila matarajio yangu, ilipofika Mei 2, 2013 mwajiriwa mwenzangu aitwaye Ahmed alifika ofisini kwangu na kuniarifu ya kwamba naitwa na Mkurugenzi Ally Edha, ilikuwa saa 11:30 za jioni Alhamisi na bila kusita nikaongozana naye hadi kwa Ally Edha nikifahamu naitwa kwa ajili ya kazi kiofisi.
“Nilishangaa nilipofika tu ofisini kwake akahitaji simu yangu, nikampa mara akamuagiza stafu mwingine aitwe Fahim akafuate laptop yangu na vifunguo ya gari yangu ofisini kwangu na ofisini kwake tulipobaki mimi, yeye na Ahmed. Alianza kunitukana na kuniambia mimi ni mwizi nimemwibia dola milioni 10 za Marekani (Sh bilioni 16).
Mara ilipoletwa laptop yangu na funguo za gari akanichukua na kuniagiza nimfungulie e-mail yangu. Nilikataa na kumwambia hii ni mail yangu binafsi na siyo ya ofisi yake, siwezi kufungua pana kazi za wateja wangu wengine (mimi ni mhasibu wa wengi). Akanitishia kunipeleka Polisi, nami nikamkubalia.
“Mheshimiwa, tukifuatana na wafanyakazi wake wengine, Ahmed, Fahim, yeye na K.V Choudry, tulishuka chini na kuingizwa katika gari ya Ahmed. Gari ikawashwa na mara akamuagiza dereva Ahmed lile gari tulilopanda lipelekwe godown (ghala) ili abadilishe gari kwenda Polisi. Cha kushangaza nikaamrishwa nishuke pale godown na kuingizwa ndani, pamoja na wale tuliofatana nao. Nilishangaa kuwakuta wengine wawili (yeye Ally Awadh anadai ni mabaunsa wake) wanaitwa Waitey na mwingine ni Abeid.
Mabaunsa waanza kumlawiti
“Mheshimiwa, wakajumuika pamoja wakanivua nguo, wakanilawiti. Wakanipiga sana kwa kutumia nondo, mikanda mizito, makonde ya nguvu na huku huyo mtumishi mwenzangu Ahmed akiwa ameielekeza pistol (bastola) kichwani kwangu kwa kuniambia leo ni kifo changu endapo nitakataa kuyakubali anayotaka bosi wake, yaani Ally.
“Mheshimiwa, mateso haya yalikuwa zaidi ya masaa mbili na nusu (zaidi ya saa mbili na nusu) nikilazimishwa nikubali kutoa kila kitu changu (assets) nimpatie yeye, vinginevyo wataniua na wakanionesha picha za maiti wawili zilizokuwepo katika simu ya baunsa wake akidai (Ally) angeniua kama hao, na kunifunga katika mfuko wa plastiki na kunipeleka shambani kwake Soga kunizika.”
Mlalamikaji anaendelea kumweleza Waziri Mkuu kwamba kutokana na mateso makali na vitisho alivyopewa, alilazimika kukubaliana na maelekezo aliyopewa, yote hiyo ikiwa ni mbinu ya kunusuru uhai wake.
Apigwa picha akiwa uchi

“Ndipo Ally Edha akanipiga picha nikiwa uchi na kusema endapo nitaenda Polisi, yeye atazitoa hizo picha kwenye mitandao ya intaneti kunidhalilisha. Hivyo nikapewa shati langu nivae na kupelekwa ofisini kwake na kulazimishwa niandike kukubali kwamba vitu vyangu vichukuliwe,” anasema.

Kwa mujibu wa mlalamikaji, mali zilizochukuliwa ni:

A: Nyumba yangu na mke wangu iliyopo Nairobi, Kenya
B: Gari zangu mbili (i) Toyota IST T786 BZG (ii) Toyota Fortuner T503 BQC
C: Bastola yangu 6mm niliyonunua Mzinga.
D: Fedha taslimu dola 100,000 (Sh zaidi ya milioni 160)
E: Mkataba wangu wa nyumba na duka (vyangu) vilivyoko Uhuru Heights
F: Ofa zangu tatu za viwanja Kigamboni

Asainishwa kwa nguvu
“Ndipo nikasainishwa; na majira ya saa 3 za usiku wakanitia katika gari aina ya Navara nyekundu mali ya kampuni –dereva akiwa Ahmed wakiwamo mabaunsa wawili, Ally Edha, na mimi. Hadi nyumbani kwangu Upanga.
“Mheshimiwa, inasikitisha kwa sababu mke wangu alipopiga simu nikiwa kwa Ally alinilazimisha niongee na mke wangu kwa lugha ya Kiingereza, na siyo Kihindi. Alikuwa anapiga kwa kutoamini kwa nini niongee Kiingereza badala ya Kihidi hadi simu ikaisha pesa ndipo tulipofika tukamkuta yupo chini anangoja aletewe vocha na mlinzi.
“Wakanibadilisha shati na kunivisha la Abeid (langu lilijaa damu). Wakamweka chini ya ulinzi mke wangu. Tukapanda juu nyumbani hadi sitting room wakamnyang’anya simu na kumkalisha chini. Ally Edha akanilazimisha nimpeleke bedroom (chumba cha kulala), ndiye akazichukua documents (nyaraka) zote na hizo pesa na mara wakaingia Choudry, Sree Kumar na Ramana ambao wote ni wafanyakazi wake; na ni Wahindi wakiwa na laptop na printer.
“Ghafla wakiwa na hizo laptop huyo Choudry na Kumar wakaelekezwa kuandika maneno ya mkataba ambayo mimi na mke wangu tukalazimishwa kuweka sahihi zetu kukubali kuzitoa mali zetu kwa huyo jambazi Ally. Nakumbuka hata watoto wanalia kutaka maziwa nyumbani Ally Edha alizuia wasipewe.”
Mlalamikaji anaendelea kusema kwamba akiwa na maumivu makali, Ally Edha alitaka siku ya pili amtolee pesa katika akaunti yake iliyopo katika Benki ya STANBIC, Tawi la Nyerere Road; na akasema angezifuata hizo fedha siku ya Jumamosi.
“Alizijua hizo fedha kwa sababu ni akaunti niliyoitumia kuweka pesa za mshahara. Mshahara wangu ulikuwa Sh. milioni 6 kwa mwezi. Kama hilo halikutosha, alikuta chumbani kwangu vitabu vitatu vya hundi za akaunti ya pamoja na mke wangu; Standard Chartered (Nairobi, 2), Benki ya Exim (3), Benki ya NBC, akatulazimisha tuzitie sahihi zetu- na tukafanya hivyo.”
Mlalamikaji, mkewe waonywa watauawa
“Siku hiyo aliniambia mimi na mke wangu kwamba kama angesikia tumemueleza mtu yeyote haya mambo, angetuua. Kweli tukaogopa sana hadi siku ya tarehe 4, 2013 ndipo alipomtuma Sree Kumar kuja kuchukua zile milioni 22 alizoagiza nizitoe katiba akaunti yangu ile siku ya tarehe 2 Mei 2013. Nilimkabidhi Sree Kumar akampelekea Ally Awadh.
“Mheshimiwa, nakumbuka namna tarehe 8 Mei, 2013 Choudry (Mfanyakazi wa Ally Awadh) alinitumia meseji mbili kwa kutumia simu yake kwamba angependa aje nyumbani waniletee pochi waliyochukua siku ya tukio nyumbani kwangu ambayo ni ya mke wangu yenye kadi yake ya ATM na kopi ya leseni ya udereva. Nikawaambia sitokutana nyumbani, tukapanga anikute Mtaa wa Morogoro/Jamhuri akaleta akanikabidhi bila ya kunisalimu.”
Danadana za Polisi Oysterbay
“Mheshimiwa Waziri Mkuu, siku ya Jumamosi tarehe 4 Mei 2013 nilipatiwa wakili aitwaye Mwanganga. Nikamueleza, akaamua tukamuone RPC Kova (Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam). Tulifika saa za mchana, nikamueleza na nilipotaka kumwonyesha majeraha yangu alikataa na kusema kuangalia majeraha sio kazi yake ila alipiga simu Oysterbay akatuagiza twende. Tukafuatana na wakili hadi Oysterbay.
“Mheshimiwa, hiyo tarehe 4 Mei 2013 tulifika Oysterbay tukamuona ofisa mmoja simfahamu jina ila sura namfahamu (wakili wangu anamfahamu). Hakuonekana kujali sana, ndipo akatupeleka ofisi nyingine (wakili anaifahamu). Hapo huyo askari akamuita mama mmoja polisi ndipo akatupeleka ofisi nyingine, ofisa akamuagiza andike maelezo naye akanisikiliza na akanipeleka kwa ofisa mwingine. Huyo ndiye aliandika maelezo yangu.
“Cha kushangaza huyo ofisa alianza kusema ‘wewe tayari umetajwa kwenye kesi nyingie ya Lake Oil’, lakini tukamwambia aandike maelezo yangu. Yeye alidai ‘pana Mhimdi mmoja, Mukesh ambaye ni Internal Auditor (Mkaguzi wa Ndani) wa Lake Oil yupo ndani rumande hapo, na wewe pia unapaswa uwekwe ndani’. Lakini huyo ofisa na mwanasheria wangu walitoka nje. Cha kunishangaza wakili akanimbia eti inatakiwa niweke dhamana nikatibiwe ili Jumatatu nirudi au nipelekwe kutibiwa nirudishwe rumande. Lakini wakili baadaye alinifahamisha wameyamaliza- kampatia Sh 100,000; hivyo ningepaswa nimrejeshee hizo pesa.
“Hivyo statement (maelezo) iliandikwa na nikapewa medical examination report yenye case file no. OB/RB/7853/2013 ya tarehe 4 Mei, 2013. Ndipo nilipoenda Sinza Hospitali kwa matibabu.”
Woga wamfanya akimbilie Zanzibar

Mlalamikaji anasema kutokana na woga wa ahadi za mateso zaidi au kuuawa kama alivyoahidi Awadh, aliamua Mei 5 aende mafichoni Zanzibar.

“Tarehe 6 Mei nilipigiwa simu na Mutafungwa aliyejitambalisha kwangu kwamba yeye ni OCD wa Kinondoni akisema amesikitishwa kuisoma statement yangu na angependa kukuona. Hivyo nikarejea Dar es Salaam na tarehe 7 Mei nikaenda na kaka yangu na wakili wangu. Tukamwona, akaagiza kwa ofisa mwingine wa CID kumweleza hiyo kesi ni ya ukweli kwa hiyo wakamatwe wahusika mara moja na kuniagiza nishirikiane naye.
“Baada ya siku mbili, yaani Mei 9, nikapigiwa siku na Salum (CID Osysterbay) akanieleza yeye ndiye mpelelezi wa kesi yangu na angependa kuniona. Tahere 12 Mei nilimuona Salum. Kwa sababu ya kuwa Zanzibar ndiyo maana nilichelewa kumuona. Akanisikiliza na kusema angepeleleza hiyo kesi na angeniita.
“Mheshimiwa, kila mara huyu Salum hakunipa msaada ipasavyo kwa madai kwamba hajamuona Ally Edha. Nilishangaa sana sababu ofisi ya Ally Edha ipo, wanaijua na iweje waseme hawamuoni? Baada ya muda, katikati ya Mwezi wa Ramadhani, Salum aliniita na kuniambia mwenzake aitwae James angeweza kunisaidia kuipata silaha yangu kutoka kwa Ally na nikamuona huyo James ambaye aliahidi Ally Edha akirudi safari yake kwa asilimia 90 nitapata pistol (bastola) yangu. Akasisitiza pia akimuona siku ya kwanza tu Ally angenipatia hiyo bastola.”
Aombwa chochote akishasaidiwa
“Nakumbuka katikati ya Oktoba, mwaka jana Salum alinipigia simu akasema James anauliza endapo akinisaidia kuipata hiyo bastola mimi ningempa zawadi gani. Nikamjibu, ‘Nitampatia anachotaka’ ilimradi nipate bastola na vitu vyangu.
“Mheshimiwa, Nashangaa tangu wakati huo walipoanza kutaka chochote kwangu, hawajanipigia tena, wala kunisaidia.

Nami nilishajiandaa kuwakamatisha kwa rushwa. Nikaendelea kupata matatizo ya kujificha kwa kuamini Ally Edha ana mamlaka ndani ya Jeshi la Polisi na anaweza kunifanyia chochote atakacho.
“Mheshimiwa, Nikashauriwa niende kutoa taarifa Makao Makuu ya Polisi (wizarani). Hivyo tarehe 27 Novemba, mwaka jana nilienda huko nikamuona Bwana Laizer ambaye ni Kamishna. Nikamueleza na nikamuonesha vielelezo. Alisikitika sana na hapo alimuagiza RPC wa Kinondoni ashughulikie hilo jambo na amueleze kwa kila kinachoendelea.
“Hadi leo tarehe 29 Novemba, nimeamua nikatumie barua hii na vielelezo vyangu ili unisaidie, kwani polisi hawanisaidii tangu nifanyiwe unyama huu. Najiuliza na kujiona mkiwa kwa kuamini kwamba huyu Ally Adha Awadh yupo juu ya sheria? Iweje polisi wamlinde tangu Mei 2013 hadi leo pasipo kukamatwa? Mheshimiwa Naomba msaada wako.”
Barua hii ya mlalamikaji aliweza kupeleka nakala kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Waziri wa Katiba na Sheria, Waziri wa Utawala Bora, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), na Mkurugenzi Mkuu wa Usalama wa Taifa.
Kwa upande wake, Awadh amegoma kuzungumza na JAMHURI. Mara kadhaa amepigiwa simu yake, lakini amekataa kuzungumza hata pale simu ilipopokewa. Ametumiwa ujumbe kwa nyakati na siku tofauti, lakini hadi tunakwenda mitamboni alikuwa hajajibu.
Ujumbe mmoja ulisema, “Habari za kazi.

Hapa ni gazeti JAMHURI. Tuna habari za kesi ya … dhidi yako. Tunaomba kujua kama hili suala unalijua kabla hatujaichapisha. Tangu jana tunaomba utupatie majibu- bila mafanikio. Tumetekeleza wajibu wetu kitaaluma kwa hiyo hatustahili lawama. Mhariri”. 

CHANZO: Gazeti la Jamhuri
TUPE MAONI YAKO HAPA:
LIKE PAGE YETU ILI UPATE HABARI ZAIDI

0 comments:

Post a Comment