Wakati vita ya kupambana na biashara ya dawa za kulevya ikiendelea nchini, wasafirishaji wa dawa hizo wameanza kutumia fukwe ndogondogo za bahari nchini kuziingiza kutoka Mashariki ya mbali, gazeti hili limebaini.

Januari 10, mwaka huu saa 6:30 usiku, mwandishi wetu alishuhudia mzigo unaoaminika kuwa ni dawa za kulevya, ukishushwa kutoka kwenye boti, eneo la Salender Bridge, nyuma ya Kituo cha Polisi kilichopo eneo hilo.

Baada ya boti hiyo kutia nanga, walishuka watu zaidi ya 10; Wazungu wawili, Waafrika kadhaa na mmoja mwenye asili ya Asia na kuungana na wengine wanne ambao tayari walikuwa katika eneo hilo wakiwa ndani ya magari mawili.

Mara moja walianza kupakua mizigo iliyokuwa imefungwa kwenye maboksi na kupakia kwenye magari ambayo yalikuwa yameegeshwa mbali kidogo na ufukwe huo. Kazi hiyo ilichukua muda usiozidi nusu saa na baada ya mizigo kupakiwa, magari hayo moja likiwa ni Land Cruiser liliondoka na kuelekea upande wa Morroco na jingine aina ya Nissan liliondoka kwenda uelekeo wa Posta Mpya.

Wakati magari hayo yakiondoka kwa mwendokasi, boti iliyokuwa na mzigo huo nayo iling’oa nanga na kuelekea katikati ya Bahari ya Hindi.

Chanzo chetu kilisema mzigo ulioshushwa ni dawa za kulevya na kwamba boti hizo ndogo hufika eneo hilo hata mara mbili kwa wiki.

Uchunguzi zaidi ulibaini kuwa dawa hizo huingizwa nchini kwa meli kubwa za mizigo, hasa zile zinazotoka Iran, Pakistan na Afganistan.

Ukamataji polisi

Mwandishi wetu aliwasiliana na polisi kuhusu njia hiyo ya kuingiza dawa za kulevya nchini na jeshi hilo kuahidi kutoa majibu baada ya kufanya ufuatiliaji. Kabla ya kutoa majibu juu ya ufuatiliaji huo, polisi ilikamata meli kutoka Iran ikiwa na kilo 201 za heroini katikati ya Bahari ya Hindi.

Msemaji wa Polisi, Advera Senso alisema kama taarifa hizo zingeripotiwa katika vyombo vya habari, ingekuwa vigumu kwa jeshi hilo kufanikisha kukamatwa kwa wahusika.

Katika wiki moja iliyopita, kilo 846 za dawa za kulevya zenye thamani ya Sh38 bilioni zimekamatwa kwenye mipaka ya Tanzania iliyoko katika eneo la Bahari Kuu, kiwango ambacho ni kikubwa katika rekodi ya kukamatwa kwa dawa za hizo.

Dawa hizo zilikamatwa kati ya Februari 2 na 5 mwaka huu. Kilo 350 za heroini zilikamatwa Februari 5 na wadhibiti wa dawa za kulevya wa Australia na kilo 265 za heroini zilikamatwa na wadhibiti wa kimataifa wa Canada, zote zikiwa zinaelekea Tanzania.
TUPE MAONI YAKO HAPA:
LIKE PAGE YETU ILI UPATE HABARI ZAIDI

0 comments:

Post a Comment