MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu leo, imewahukumu kifungo cha miaka mitatu jela aliyekuwa Waziri wa Fedha na Uchumi, Bazil Mramba na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona baada ya kuwatia hatiani kwa makosa mawili.
Akizungumzia
hukumu hiyo, Wakili wa washtakiwa hao, Peter Swai, amesema kwamba
hukumu hiyo imetolewa na jopo la majaji watatu ambao ni Jaji Samu
Rumanyika, Jaji John Utamwa, pamoja na Hakimu Saul Kinemela, ambapo
mtuhumiwa wa tatu wa kesi hiyo ambaye ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara
ya Fedha, Gray Mgonja, amekutwa hana hatia huku mawakili wa washtakiwa
wakiazimia kukata rufaa.
“Hatujaridhika
na hukumu ila shauri limesikilizwa na Mahakimu wa tatu. Na kwa mujibu
wa sheria tukikata rufaa aidha watakubali wote watatu au mmoja wao
atakataa, kwahiyo iwapo mmoja wao atakataa na wawili wakikubaliana hiyo
ndiyo hukumu ya Mahakama, na hicho ndicho Mahakama ilichofanya leo, hili
ni jambo la kisheria kama tunaamini kwamba uamuzi uliotolewa hauendani
na sheria tutakata rufaa kwenye Mahakama ya juu na itatafsiri sheria
upya na sisi tutapata majibu” amesema Swai.
Kwa
mujibu wa sheria ya makosa ya jinai, kosa la matumizi mabaya ya
madaraka adhabu zake ni kulipa faini ya Sh. milioni 2 au kifungo cha
kati ya mwaka mmoja au miaka mitatu jela baada ya mshtakiwa kupatikana
na hatia.
Katika
mashtaka hayo ilidaiwa kuwa washtakiwa wakiwa watumishi wa serikali,
Oktoba 10, mwaka 2003 walikaidi ushauri wa Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA) wa kuwataka wasitoe msamaha kwa Kampuni ya Alex Sterwart
(Assayers) Government Business Corporation.
Novemba
25, mwaka 2008, washtakiwa hao, walifikishwa katika mahakama hiyo mbele
ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Hezron Mwankenja, na kusomewa mashitaka 13,
likiwamo la matumizi mabaya ya madaraka. Kesi hiyo ilipangiwa jopo hilo
na kuanza kuisikilizwa mapema mwaka 2009.
Kumbukumbu
zinaonyesha kwamba katika mashitaka yaliyokuwa yanawakabili washtakiwa
ni pamoja na kudaiwa kati ya Agosti mwaka 2002 na Juni 14 mwaka 2004
Jijini Dar es Salaam, washitakiwa wakiwa watumishi wa umma kama Mawaziri
walitumia vibaya madaraka. Mramba na Yona wanadaiwa kuwa kati ya Juni
2003 na Mei 2005, wakiwa na nyadhifa hizo za uwaziri kwa makusudi na
kutowajibika waliruhusu mkataba wa kuzuia kulipa kodi ili kuipendelea
kampuni hiyo na kuisababishia serikali hasara ya Sh. 11,752,350,148.00.
Washtakiwa
hao walikuwa wanakabiliwa na mashtaka ya matumizi mabaya ya madaraka na
kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh. Bilioni 11.7 kutokana na
kutoa msamaha wa kodi kwa Kampuni ya kukagua madini ya dhahabu ya Alex
Stewart (ASSAYERS) ya Uingereza iliyoingia mkataba wa kudhibiti madini
ambapo kwa kupitia kampuni tanzu ya Alex Stewart (ASSAYERS) Government
Business Corporation waliingia mkataba na kampuni tanzu kukagua
uzalishaji wa madini ya dhahabu, kinyume cha Sheria ya Manunuzi ya Umma.
TUPE MAONI YAKO HAPA:
0 comments:
Post a Comment