Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk.Willibrod Slaa, amehoji Sh. bilioni moja zilizotengwa katika bajeti ya 2013/2014 kwa ajili ya gharama za mazishi ya viongozi wa kitaifa serikali iainishe zimetumikaje kwa sababu hadi sasa hakuna kiongozi yeyote wa kitaifa aliyekufa.
Alisema hayo wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Sherui na Kengege jimbo la Iramba Magharibi mkoa wa Singida.
Alisema serikali inapaswa kutoa maelezo ya fedha hizo kwa kuwa mwaka wa fedha umekwisha sasa na hakuna hata kiongozi yeyote wa kitaifa aliyefariki hali inayotia mashaka zinaweza zikawa zimenufaisha watu wachache waliopo serikalini.
Dk. Slaa alisema ni jambo la kushangaza kutengwa kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya mazishi ya viongozi wa kitaifa huku maeneo mengi ya nchi yakikosa huduma muhimu ikiwamo wanafunzi kukosa madawati.
“Serikali inapotenga fedha kwa mazishi ya viongozi wa kitaifa utafikiri ina ahadi na mwenyezi Mungu, lazima tujenge utamaduni wa kutenga fedha kwa ajili ya mambo muhimu, leo hii kwenye mashule hakuna hata madawati wanafunzi wanakaa sakafuni,” alisema.
Alisema umaskini wa Watanzania siyo mapenzi ya Mwenyezi Mungu bali umetokana na mipango mibovu ya viongozi ambao wamekuwa wabinafsi wanapopata madaraka wanajali maslahi yao binafsi.
Naye Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, alisema serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi kwenye Halmashauri kwa ajili ya miradi ya maendeleo lakini bahati mbaya wananchi hawapewi taarifa na viongozi jinsi zinavyotumika.
Lissu alisema kutoweka wazi mapato na matumizi ya fedha za umma kumekuwa kukisababisha watendaji wa halmashauri husika kuzifuja na hivyo miradi kushindwa kutekelezwa.
Dk. Slaa amehitimisha ziara yake siku 20 kwa kuzungumza na wananchi katika majimbo yote ya mikoa ya Kigoma, Tabora na Singida.
TUPE MAONI YAKO HAPA:
0 comments:
Post a Comment